DARSA ZA SHEIKH ABDULKADER SHAREEF

KCWW RAM/10 1438

FADHILA ZA UHARAKISHA KUFUTURU II

Darasa ya Ramadhani, Jumatano tarehe 5 Ramadhani 1438, ‎sawa ‎na 31 Mei 2017‎


222 Mlango wa Fadhila za Kuharakisha Kufuturu, Sunna ya Kitu cha ‎Kufuturia na Dua ya Kusoma Baada ya Kufuturu

     1245. Imepokewa kutoka kwa Abu Ibrahim ‘Abdullah bin Abi Awfa رضي الله عنهما akisema: Tulisafiri na Mtume akiwa amefunga. Jua ‎lilipokuchwa, alimwambia mtu mmoja, “Fulani! Teremka kipando chako na ‎tupatie uji!” Yule mtu akamjibu, “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Si bora ‎ungesubiri mpaka litande giza?” ‎

Mtume akamwambia, “Teremka kipando chako na tupatie uji!” ‎Yule mtu akamjibu, “Lakini bado mchana, kweupe!” ‎Mtume akamwambia tena, “Teremka utupatie uji!” ‎Yule mtu akateremka na kuwapatia uji. Na Mtume ﷺ akanywa kisha akasema, ‎“Mkiona usiku umeingia upande huu basi wakati wa kufuturu umewadia kwa ‎mwenye kufunga” huku akionesha kwa mkono wake upande wa mashariki. _Muttafaq ‘alayhi.

     1246 Imepokewa kutoka kwa Salman bin ‘Amir Adh-Dhwabbiyy As-‎Swahaabiyy رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume , ‎“Anapofungua mmoja wenu afungue kwa tende, akikosa tende basi afungue ‎kwa maji, kwani maji ni kinywaji safi”. Ameipokea Abu Daud na Tirmidhi aliyesema  ‎Hadithun hasanun Swahih.

     1247. Imepokewa kutoka kwa Anas ‎رضي  الله عنه ‏ akisema: “Ilikuwa ‎kawaida ya Mtume kufuturu kabla ya kuswali, kwa vijitende ‎vilivyoiva (yaani bado kunyauka), zikikosekana basi hufuturu kwa tende kidogo ‎‎(tende za kawaida zilizonyauka), zikikosekana basi hufuturu kwa vijifundo ‎viwili vitatu hivi vya maji”. Ameipokea Abu Daud na Tirmidhi aliyesema  Hadithun ‎hasan.

UFAFANUZI

Hadithi za sehemu hii, kama hadithi zilizotangulia, zinatilia mkazo wakati ‎wa kufuturu, kuharakisha kufuturu, na kufuturu kwa kitu gani. ‎

Kwanza, jua likishakuchwa tu, basi wakati wa kufuturu ‎umeshafika, hata kama bado kuna mwangaza angani. Kigezo ni kuchwa jua, si ‎kutanda weusi au giza. Kwa maana hiyo, ukiwa na ala au chombo cha ‎kuaminika, kinachokupa ishara ya kuwa jua limekuchwa, kama saa madhubuti, ‎basi wakati wa kufungua kinywa umefika, maana kigezo ni kuchwa jua, si ‎kutanda weusi au giza angani. ‎

Pili, ukishahakikisha kuwa jua limekuchwa, basi jambo la ‎kwanza kufanya ni kufungua kinywa. Acha mengine yote ufungue kinywa kwanza. Hiyo ndiyo Sunna ya Mtume na amri yake. ‎

Tatu, kama una tende, basi fungua kwa tende, kama huna basi tunda ‎lolote tamu au kitu chochote kile kitamu. Kikikosekana basi hata glasi ya maji, ‎kwani maji yanasafisha vitu vingi mwilini. Hiyo ni Sunna ya Mtume ‎. ‎

Nne, Sunna ya Mtume ni kufuturu kwanza, kisha kuswali ‎magharibi, na si kinyume chake. ‎

Mwisho, kuomba dua baada ya kufungua kinywa, kwani Mtume ﷺ amesema: “Dua ya mwenye kufunga hairudi mikono mitupu”. Muttafaq alayhi. ‎

Miongoni mwa Dua ziliyopokewa kutoka kwa Mtume ni:
اللهم لك صمت وعلى رزقك افطرت  ذهب الظمأ، وابتلت العروق، وثبت الأجر إن شاء الله
‎“Ewe Mola wangu! Kwa ajili Yako nimefunga, na kwa riziki Yako ‎nimefungua. Kiu kimeondoka na mishipa imerutubika, na ujira, kwa utashi ‎wa Allah, umepatikana!”‎

YALIYOMO NA YATOKANAYO

1. Kuharakisha kufuturu ni Sunna ya kauli na vitendo vya Mtume .
2. Sunna kufuturu mara tu baada ya kuhakikisha kuwa jua limekuchwa.
3. Kuchwa jua ndio kigezo cha kumalizika Swaumu ya Siku.
4. Kujuzu kufuturu kwa uji na mfano wake, ikikosekana tende.
5. Kufuturu kwa kokwa mbili tatu za tende ndiyo Sunna.
6. Ikikosekana tende, au tunda tamu, basi fungua kinywa kwa mafundo ‎mawili matatu ya maji.
7. Tende ina virutubisho vingi vya kuchangamsha nguvu mwilini, hasa kwa ‎mwenye kufunga.
8. Maji yana faida kubwa mwilini, hasa wakati wa kufuturu.
‎9. Kujuzu kufunga ukiwa safarini.
10. Kujuzu kutoa ushauri kwa Mtume hakumaanishi kumpinga.
11. Riwaya nyengine zimefafanua kuwa aliyetoa ushauri huo alikuwa ‎Sayyidina Bilal bin Rabah  رضي الله عنه.
12. Mapenzi na hima ya Sayyidina Bilal رضي الله عنه kwa Mtume na mapenzi ‎ya Mtume kwa Sayyidina Bilal رضي الله عنه.
13. Kujuzu kuwa na mtumishi msaidizi safarini.
14. Sunna ni kufuturu kwanza, kisha kuswali.
15. Umuhimu wa kufuata Sunna za Mtume kwa kauli na vitendo.‎

INAENDELEA ...

والله أعلم وبالله التوفيق‎ ‎
الحقير إلى الله تعالى الدكتور السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم


Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka “Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi ‎wa ‎Umma”, kitabu ‎ambacho ni tafsiri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإمام ‏النووي ‏‎ ‎kilichotungwa na Imam An-Nawawi na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com
NiNimeulizwa pembeni na watu wawili tofauti, na nimewajibu pembeni, ila kwa faida ya watu wengi nimeona nitoe swali na jibu hadharani.
Nanukuu:
Salaam Alaykum Sayyid.
Nipe tafauti ya Sala ya Tahajud na sala ya Kiyamul lail
Nini Fadhila za Tahajjud na Qiyaam al-Lyl?
JIBU.
BISMILLAH.
Ibada yoyote, isiyokuwa ya Faradhi, inayofanywa usiku, baada ya Kuswali Ishaa na kabla ya kuchomoza alfajiri, ni Qiyaam al-Layl. Hivyo basi, قيام الليل maana yake kusimama usiku kwa ibada, au kuhuyisha usiku kwa ibada, kwa ajili ya Allah peke Yake.
Na kusimama usiku au kupitisha Usiku, siyo lazima usiku mzima au hata mwingi wake. Bali hata sehemu, tu, ya Usiku, hata kama ni masaa machache au saa moja hivi au hata nusu saa tu, kwa kufanya Ibada kama Kuswali Sunna, Kusoma Qur’ani, Kumtaja Mwenyezi Mungu, Kusoma ilimu ya Dini, kama Hadithi na Tafsiri na kadhalika. Na kila muda wa kufanya Ibada hizo unapoziidi kuwa mrefu ndipo na thawabu za Qiyaam al-Layl nazo zinapozidi na kuongezeka; na Hivyo Qiyaam al-Layl kina faida zaidi.
Kwa maana hiyo, yule aliyefanya Ibada usiku, kwa muda mrefu zaidi, ndiye mbora wa wanaofanya Qiyaam al-Layl. Na yule aliyefanya Ibada usiku, kwa muda mchache zaidi, hata kama muda wa nusu saa tu, basi ni mbora wa watu wote ambao hawakufanya ibada usiku.
Kwa maana hiyo, Qiyaam al-Layl ni ibada inayofanya usiku, na ambayo SI FARADHI.
Kwa mfano, Swala za Witri, kuanzia rakaa moja hadi kuendelea mpaka kufika 33, au 37 kwa kuziswali rakaa mbili mbili, na kumalizia rakaa moja. Au Tarawehe katika mwezi wa Ramadhani. Vivyo hivyo, Kusoma Qur’ani, iwe ndani ya Swala hizo za Sunna, au nje ya Swala hizo. Kumtaja Mwenyezi Mungu; yaani kusoma nyiradi mbali mbali. Kujifunza ilimu za Dini, kama Tafsiri na Hadithi za Mtume صلى الله عليه وسلم .
Huko ndiko kufufua au kuhuyisha au kusimama kwa Ibada Usiku, vile watu wengine wamelala fofofo wanakoroma.
Ama Tahajjud maana yake Swala ISIYOKUWA YA FARADHI, na ambayo inaswaliwa Usiku, BAADA ya kulala na kisha kuamka kwa Ibada hiyo au hizo. Kama Witri na Tarawehe.
Kwa maana hiyo, kila mwenye Kutahajjad (amelala kidogo baada ya kuswali Isha, kisha akaamka na kuswali swala za usiku) anaingia katika fadhila za Kusimama Usiku; lakini SI kila anayesimama usiku kufanya Ibada ni Mutahajjid.
Hivyo basi, kulala usiku –baada ya kuswali swala zako za faradhi (Mgharibi na Isha), kisha ukaamka kwa kufanya Swala za usiku, unakuwa UMETAHAJJAD na UMESIMAMA USIKU KUFANYA IBADA. Na mtindo huu ndio uliokuwa HULKA ya Mtume صلى الله عليه وسلم (ingawa inafaa tutambuwe kuwa Tahajjud kwa Mtume صلى الله عليه وسلم ILIKUWA WAJIBU KWAKE, YAANI KAMA FARADHI kama alivyoamwishwa na Allah afanye hivyo katika Surat al-Muzzammil, 1-6.)

Mtume صلى الله عليه وسلم alikuwa akifanya Ibada za Usiku, na kusimama kuswali swala ndefu, yaani kusoma Sura ndefu (Wakati mmoja alisoma Surat al-Baqara, Akaingia al-Imraan, akaingia al-Nisaa, katika Rakaa moja tu, kiasi kijana aliyjaribu kumfuata nyuma yake, alikaribia kumuacha akae kitako) na kuomba dua kwa muda mrefu, katika sijida, hata ikawa miguu yake inamvimba, na kutokwa na melengelenge, licha ya kwamba ameahidiwa na Mola wake kufutiwa dhambi zake zilizopita - na za baadae! (Bukhari)
Alipoulizwa na Bibi Aisha رضي الله عنها kwanini anafanya hivyo (kurefusha Swala, kwani angeliweza kuswali rakaa chache fupi tu), licha ya ahadi aliyopewa na Mola wake, alijibu kwa kusema: “Na kwanini nisiwe mja mwenye kushukuru!” (Muttafaq Alayhi)
Yaani “nataka niwe mja mwenye kumshukuru Mola wake. Kwa sababu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: Mkinishukuru basi Naapa nitawaongezeni!” صلى الله عليه وسلم nani kama yeye, amjuaye Mola wake na kumuabudu kikomo cha kumuabudu!
Mmoja wapo wa maswahaba wa Mtume صلى الله عليه وسلم anayeitwa al-Hajjaj bin ‘Amr al-Answari رضي الله عنه alikuwa akisema kuwambia watu:
“Hivi mnafikiri kwamba mtu akisimama kidogo usiku akaswali ndiyo ameshakuwa MUTAHAJJID! Waapi! Tahajjud ni kuswali baada ya kulala, na kisha kulala tena na kuamka na kuswali tena. Na hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume صلى الله عليه وسلم (al-Talkhiis, cha Ibn Hajar, juzuu ya 2, ukurasa 35) Hadithi hiyo ameipokea Tabarani.
Swala yoyoteya SUNNA inayoswaliwa usiku, au Dua yoyote inayoombwa usiku ni Quyaam al-Layl, na iwapo utalala baada ya Isha kisha ukaamka mahasusi kwa kuswali SUNNA za Usiku, -kama Witri- kabla ya kuchomoza alfajiri ni TAHAJJUD na, wakati huo huo
ni QIYAAM AL-LAYL.
Kwa ufupi, Qiyaam al-Layl ni Ibada YOYOTE ifanywayo Usiku, sawa sawa uifanye kabla ya kulala, au ulale kisha uamke ufanye ibada hizo, kisha urudi tena au usirudi tena kulala, na kusubiri Swala ya Alfajiri.
Kuna Dua nyingi zilizopokewa kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلم za kuomba usiku, iwe ndani ya swala ua nje ya swala. Nyingi ya dua hizo zimo kwenye kitabu cha al-Adhkaar cha Imam al-Nawawi رحمه الله na nyengine katika vitabu vya Hadithi, kama al-Targhiib wa al-Tahiib, cha Imam al-Mundhiri.
Na kuna Aya za Qur’ani na hadithi chungu nzima, zinazo zungumzia Fadhila za Qiyaam al-Layl na Tahajjud.
Kwa mfano. Mwenyezi Mungu Amewasifu wachamungu, katika Surat al-Dhariyaat kwa kusema: “Hakika wachamungu watakuwa katika mabustani yenye chemchemi. Wanapokea aliyowapa Mola wao. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghafira. Al-Dhariyaat: 15-18
Na amesema: “Hakika wanao ziamni Aya zetu ni hao tu ambao wankikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na kumsabihi Mola wao kwa kumshukuru, na hawajivuni. Mbazo zao zinaachana na matandiko kwa kumwomba Mola wao, kwa khofu na matumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku. (al-Sajda: 15-16)
1. Imepokewa kutoka kwa Jabir رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume صلى الله عليه وسلم Katika kila Usiku, huweko saa moja, ambayo iwapo mja Mwislamu atamuomba Allah, katika saa hiyo, jambo lolote lile la kidunia ua la Akhera, basi Atampa tu. Na saa hiyo imo katika kila usiku” Ameipokea Muslim, H.757.
2. Imepokewa kutoka kwa Abu Umama al-Bahiliyy رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume صلى الله عليه وسلم “Jitahidini kusimama Usiku (kwa ibada) kwani huo ndio mtindo na hulka ya Waja wema waliokutangulieni, na ndiyo njia ya kujisogezeni karibu zaidi kwa Mola wenu, na ndiyo kifutio kikubwa cha dhambi, na kiokozi cha kuepuka dhambi” Imepokewa na Tirmidhi, H.3549, Ibn Abid-Dunya, Ibn Khuzayma, na al-Hkim, Juzuu 1, H.308.
3. Imepokewa kutoka kaw Abu Hurayra رضى الله عنه akisema: Amesema Mtume صلى الله عليه وسلم Funga iliyobora kabisa kuiko funga zote ni Funga ya Rmadhani, na Swala iliyobora kabisa, baad ya Swala za Faradhi, ni Swala za Usiku.” Muslim, H.1163; Abu Daud, H.2429; Tirmidhi, H. 740; na Nasai, H.207.
4. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Sallam رضى الله عنه akisema: Alipokuja Madina Mtume صلى الله عليه وسلم watu walitoka makundi kwa makundi kwenda kumlaki, na mimi nilikuwa miongoni mwao. Basi nikauangalia uso wake kwa umakini mkubwa sana, na nikatongoa (kuelewa na kufahamu kwa undani kabisa) kuwa kamwe hawezi kuwa mtu mwongo!.Na kauli yake ya mwanzo niliyoisikia kutoka kwake ni: “Enyi wanaadamu! Toleanieni Salama (salimianeni), na wakirimuni watu chakula, na shikamaneni na ndugu na jamaa zenu, na Swalini Usiku – vile watu wamelala- mkifanya hivyo mtaingia Peponi kwa salama” (hakuna kuhesabiwa) Tirmidhi, H. 2885; Ibn Majah,H.3251; al-Hakim, 3\12.
5. Imepokewa kutoka kwa Asmaa’ bint Yazid رضي الله عنها akisema: Amesema Mtume صلى الله عليه وسلم “Watafufuliwa Watu katika Janwa moja, Siku ya Kiyama. Na kutanadiwa (Wataitwa) “Wawapi waliokuwa wakiinua mbavu zao kutoka kwenye matandiko yao (ya kulalia)?” Basi watatokeza, na watakuwa watu wachache tu (kulingana na umati wa watu). Basi wataingizwa Peponi pasi na kuhesabiwa, na waliosalia wataamrishwa kuelekea kwenye sehemu ya kuhesabiwa (kwa amali zao). Al-Bayhaqi, Shu’ab al-Iiman, H. 3244. Al-Targhiib wa al-Tarhiib:H.9\901
Kwa maana hiyo, swala maalum, ambayo inaswaliwa muda maalum, tena usiku, huitwa Tahajjud. Kama Witri na Tarawehe. Swala hizi mbili zinaswaliwa Usiku tu. Vile Witri inaswaliwa kila siku usiku baada ya isha, Tarawehe inaswaliwa usiku baada ya Isha katika Mwezi wa Ramadhani. Ndiyo maana Swala hizo mbili hazikimiwi, kama Iqama ya Swala za Faradhi, bali hunadiwa tu: Swalaatul-Layl, al-Swalaatu Jaami’ah, iwapo inaswaliwa jamaa.
Ama mtu akiswali peke yake, basi hakuna haja ya kunadi chochote, anasimama na kuswali Witri zake au Tarawehe peke yake, katika mwezi wa Ramadhani.
Na Tahajjud na Qiyam al-Layl LAZIMA zifuatiwe na Swala ya Alfajiri. Hakuna sababu kuswali Sunna za usiku, lakini ikiingia alfajiri unakwenda kulala.
Au unaamka kwa Thajjud kisha unakwenda kulala huamki kwa Swala ya Alfajiri. Tahajjud yako haina faida, kwako, na qiyaam al-Layl yako, vile vile, haina faida.
NYONGEZA. Tahajjud au Qiyaam al-Layl ni Sunna ya kudumisha, kadiri ya uwezo wa mtu. Si Sunna ya kufanya mara moja moja. Hivyo, kama unataka kuingia katika watu wanaohesibaiwa Mutahajjiduun au Wanao Simama usiku kumuabudu Allah na kufanya ibada, basi bora ama uswali rakaa chache unazoweza kudumisha kila siku usiku, au ibada yoyote ile ambayo utaweza kuidumisha, kadiri ya uwezo wako. Hata kama utalala, kisha uamke na kuswali RAKAA MOJA TU YA WITRI, basi wewe ni Mutahajjid na Umesimama Usiku kwa Ibada.
وبالله التوفيق
الحقر عبد القادر شريف آل الشيخ





Hadithi za Leo, Jumaane tarehe 6 Mfungo Nane, 1437 sawa na 16 February, 2016.
SEHEMU YA TATU KUHUSU KUJICHUNGA.
1- Mlango wa Kujichunga (kujidhibiti)
Amesema Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالي :
1. [Mwenyezi Mungu] Anaye kuona unapo simama, na mgeuko wako miongoni mwa wenye kusujudu” (al-Shu’araa: 218-19)
2. Na Yeye, Yu pamoja nanyi popote mnapokuwepo (al-Hadiid:
3. Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki kitu Kwake, duniani wala mbinguni (al-‘Imraan:5)
4. Hakika Mola wako Mlezi Yupo kwenye mavizio Anawavizia (al-Fajr: 14)
5. Anajuwa khiyana ya macho na vilivyo ficha vifua (al-Ghafir:19)
66. Sita: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume صلي الله عليه وسلم :
“Kulitokea watu watatu wa qawm ya Bani Israil: mmoja alikuwa mkoma, wa pili alikuwa kipara na wa tatu alikuwa kipofu.
Mwenyezi Mungu Aliwajaribu. Aliwatumia malaika, aliyemwendea mkoma na kumuuliza: “Kitu gani ndicho unachokipenda sana?
Akajibu: “Rangi nzuri na ngozi nzuri, na kuondokewa na kinacho wafanya watu waninyanyapae”
Yule Malaika akampangusa na hivyo maradhi yakamuondoka na akapewa rangi nzuri. Yule Malaika akamuuliza tena: “Utajiri gani unaupenda zaidi?”
Akasema: “Ngamia au ng’ombe (aliyepokea Hadithi hakumbuki yupi hasa). Akapewa na yule Malaika, ngamia jike mja mzito na kumuombea: “Mwenyezi Mungu akubariki katika ngamia huyu!”
Akamuendea kipara. Akamuuliza: “Kitu gani ndicho unachokipenda sana?”
Akajibu: “Napenda niwe na nywele nzuri, na kuondokewa na kile kinacho wafanya watu waninyanyase” Akampangusa na hivyo upara ukatoeka na kupata nywele nzuri.
Yule Malaika akamuuliza tena: “Utajiri gani unaupenda zaidi?”
Akasema: “Ng’ombe” Akapewa na yule Malaika, ng’ombe jike, mja mzito na kumuombea: “Mwenyezi Mungu akubariki katika ng’ombe huyu”.
Akamuendea kipofu na kumuuliza: “Kitu gani ndicho unachokipenda sana?”
Akajibu: “ Kurejeshewa na Mwenyezi Mungu macho yangu, ili niwaone watu”
Yule Malaika akampangusa na Mwenyezi Mungu Akamrudishia macho yake. Akamuuliza tena: “Utajiri gani unaupenda zaidi”
Akasema: “Mbuzi” Akapewa mbuzi mwenye kuzaa sana.
Wanyama wote wale wakazaana na kuzaliana.
Baadae, yule Malaika akamwendea mkoma – katika sura ya binadamu mwenye umbile na sura ya ukoma. Akamwambia: “Mimi masikini, natoka mbali na nimeishiwa na kila kitu, na hapana, baada ya Mwenyezi Mungu, ila wewe kunisaidia kufika ninako enda. Nakuomba kwa Jina la Aliyekupa rangi nzuri, ngozi nzuri na utajiri, unipe ngamia mmoja aweze kunifikisha ninako enda!”
Akamjibu: “Mimi nina majukumu mengi sana!”
Yule Malaika akamwambia: “Naona kama nakufahamu. Hivi si ulikuwa mkoma ukikimbiwa na watu na ulikuwa masikini Akakukpa Mwenyezi Mungu Alivyokupa?”
Akasema: “Hapana! Mimi nimerithi mali hizi kutoka kwa babu na mababu”
Malaika akamwambia: “Kama unasema uwongo, basi Mwenyezi Mungu Akurudishe hali uliyokuwa nayo kabla”
Akamuendea kipara, akiwa katika sura na umbo la kipara. Akamuomba kama alivyo muomba mkoma. Na kipara naye akamjibu kama alivyojibiwa na mkoma. Malaika akwambia: “Kama unasema uwongo, basi Mwenyezi Mungu Akurudishie hali uliyokuwa nayo kabla”
Akamuendea kipofu, akiwa katika sura na umbo la kipofu na kumwambia: “Mimi masikini na msafiri. Nimeishiwa na kila kitu na hakuna, baada ya Mwenyezi Mungu, ila wewe kunisaidia kufika niendako. Nakuomba kwa Jina la Aliyekupa macho, mbuzi mmoja nijisaidie naye kufika niendako.
Yule kipofu akasema: “Mimi nilikuwa kipofu; Akanurudishia macho yangu Mwenyezi Mungu! Chukua mbuzi uwatakao na saliza uwatakao kuwasaliza. Kwani, naapa kwa jina la Allah sitaona uzito wowote, kwa chochote utacho chukua kutoka kwenye mali yangu!”
Yule Malaika akamwambia: “Kaa na mali yako; kwani Mwenyezi Mungu Ameridhika nawe, na Amewakasrikia wenzi wako wawili” Muttafaq ‘alayhi.
67. Saba: Imepokewa kutoka kwa Abu Ya’la Shaddad bin Aws رضي الله عنه akisema: Amesema Mtumeصلي الله عليه وسلم :
“Mwerevu [mwenye akili] ni yule mwenye kuichunga nafsi yake na akatenda yatayomsaidia baada ya kifo. Na mvivu ni yule anaye shibisha nafsi yake matamanio yake, na [papo] akataraji kulipwa mema na Mwenyezi Mungu” Ameipokea Tirmidhi nakusema: Hadithun hasan.
UFAFANUZI.
Tunaendelea na Hadihi za mlango huu wa Kujichunga na kujlinda , dhidi ya mitihani mbali mbali inayotukabili, kila siku, katika maisha yetu; ambapo tunajaribiwa na Mwenyezi Mungu kama tutajichunga na tutajtunza kufuata Amri Zake, ili tupate Radhi Zake na Rehema Zake, au tutamsahau kutokana na kiburi na ghururi, na hivyo kustahiki Ghadhabu Zake; licha ya kujua FIKA, kwamba kila tulicho nacho kinatoka Kwake, na ametupa SI kwa uhodari wetu, wala SI kwa kutupendelea tu, dhidi ya wengine, bali kwa kutujaribu kama Tutamshukuru na hivyo Azidi kutuongezea, au tutamkufuru na hivyo Atuteremshie laana Yake: والعياذبالله .
Kupewa au Kunyimwa ni sehemu ya mitihani ya Mwenyezi Mungu kwa mja Waike. Ukitambua hilo, na ukatenda kwa kutambua kuwa umo katika Mtihani maalum, na hivyo ukashukuru na Kuomba dua, kwa kauli na vitendo, basi Aliyekutumia Mtiahni huo atakuzidishia alichokupa, au atakupa alichokunyima. Lakini ukaghurika na kumsahau aliyekufanyia mtihani huo na ukaona kuwe mwalimu ni wewe, basi atakupkonya alaichokupa, au atakuzidishia balaa alilokuteremshia. JICHUNGE!
YALIYOMO NA YATOKANAYO.
1. Mojawapo wa sifa mbaya sana, ambayo kila mtu anatakiwa ajichunge nayo ni UBAKILI na UCHOYO.
2. Ubakhili na Uchoyo, usipotahadhari, unampelekea mja kusahau Neema za Mwenyezi Mungu, bali hata kuzikana.
3. Ubakhili, ukichanganyika na Uwongo, basi Laana yake ni maradufu; kama ziliowafika Kipara na Mabalanga.
4. Ukweli na Ukarimu ni sifa njema sana kujipamba nazo.
5. Ukweli na Ukarimu, ukichanganyika na Imani, basi malipo ya Radhi za Mwenyezi Mungu ni makubwa mno.
6. Ukweli na Imani ya Kipofu ndio uliomuokoa katika Mtihani wa Mwenyezi Mungu.
7. Si kila akujiaye mbele yako ni mwanadamu mwenzako; anaweza kuwa ametumwa katika sura ya manadamu kukufanyia mtihani.
8. Malipo ya Mwenyezi Mungu, kwa mja Wake, nikwamba mujibu wa nia na matendo ya mja huyo.
9. Kujuzu kusimulia matukio ya wana wa Israil wa kale –kupitia nukuu swahihi za Mtume صلى الله عليه وسلم – kama fundisho na onyo la kujifunza kutokana na matukio hayo.
10. Ni wajibu kwa kila Mwenye kumuamini Allah na Mtume Wake, kuwa mkweli na mkarimu.
11. Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kauli na vitendo ni sababu ya kuongezewa ulichopewa, au kuondoshewa tatizo ulilopewa kwa kufanyiwa mtihani.
12. Subira na Uvumilivu, na kushukuru kwayo, ni dalili ya kupasi mtihani wa Allah juu yako.
13. Ukweli wa kutambua fadhila za Mwenyezi Mungu huonekana katika kauli na matendo ya mwanadamu, mwenye kujichunga.
14. Kutojichunga kunweza kupelekea kusema Uwongo na kuwa mbakhili, na hivyo kustahiki Laana ya Mwenyezi Mungu.
15. Asiyejifunza kutokana na matukio hana ajifunzalo.
16. Wajibu wa Mwislamu kuichunga nafsi yake, na kuwa mkali nayo, pale inapotaka kumtokomeza kwenye matamanio yake tu.
17. Mwenye akili na busara ni yule anayejishughulisha na yenye kumfaa, khasa katika maisha ya Akhera.
18. Mjinga na mpumbavu ni yule mwenye kujishughulisha na yasiyokuwa na manufaa naye; na papo akataraji Rehema na Radhi za Mwenyezi Mungu.
19. Wajibu wa kutimiza wajibu wa kumuabudu Allah, kwa kauli na vitendo, na SI kutegemea njozi na ndoto za mchana, kweupe.
20. Hatari ya kuwa mtumwa wa matamanio ya nafsi yako; kwani Nafsi siku zote inapenda maovu.
21. Adui mkubwa wa mtu ni matamanio yake mwenyewe: Shetani wa mtu ni mtu.
22. Mwenyezi Mungu humlipa mja kwa amali zake mwenywe, si kwa mujibu wa ndoto na njozi zake, bila ya vitendo.
23. Mauti hayaepukiki. Jichunge nayo!
24. Mlipo ya Siku ya Kiyama ni kwa mujibu wa Amali ZAKO. Jitayarisho ipasavyo!
INAENDELE.A.....
والله أعلم
وبالله التوفيق
الحقير عبد القادر شريف آل الشيخ

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ambacho ni tafisri kamili ya رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي kilicho tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir Shareef.
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye Whatsup na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com


Hadithi za Leo, Jumatano tarehe 7 Mfungo Nane, 1437 sawa na 17 February, 2016.
SEHEMU YA NNE KUHUSU KUJICHUNGA.

1- Mlango wa Kujichunga (kujidhibiti)
Amesema Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالي :
1. [Mwenyezi Mungu] Anaye kuona unapo simama, na mgeuko wako miongoni mwa wenye kusujudu” (al-Shu’araa: 218-19)
2. Na Yeye, Yu pamoja nanyi popote mnapokuwepo (al-Hadiid: 4)
3. Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki kitu Kwake, duniani wala mbinguni (al-‘Imraan:5)
4. Hakika Mola wako Mlezi Yupo kwenye mavizio Anawavizia (al-Fajr: 14)
5. Anajuwa khiyana ya macho na vilivyo ficha vifua (al-Ghafir:19)
68. Nane: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنهakisema: Amesema Mtume صلي الله عليه وسلم :“Miongoni mwa uzuri wa sifa ya Uwislamu wa mtu ni kuacha yasiyomhusu” Hadiithun hasan, ameipokea Tirmidhi na wengine.
UFAFANUZI Kuacha yasiyomhusu maana yake kuachana na mambo ambayo, kwa upande wa Dini na Imani yako, hayana faida wala manufaa kwako, si duniani wala si Akhera, na zaidi yasiyokuletea tija yoyote Akhera. Yaani kuachana na mambo ya kipuuzi, hata kama ni mambo ambayo hayakatazwi.
Kwa mfano, kukaa “vijiweni” au tabia ya kuropokwa ropokwa, kuzurura ovyo ovyo, na hata kukubali kuwa mhanga au muathiriwa wa janga liliozagaa enzi zetu za mitandao ya kijamii (Facebook na Instigram), ambapo mtu anapitisha muda wake mrefu sana kuperuza peruza kutafuta unabe, na kusoma mambo ya upuuzi tu. Kwa ufupi kuachana na mambo ambayo huyahitajii wala huna dharura nayo.
Ama ukiwa unayahitajia, au una dharura nayo, mfano wa kufanya maazoezi, basi uzuri wa kukamilisha sifa yako ya Uwislamu ni kuyafanya mambo hayo na si kuyadharau au kuyapuuza.
Vivyo hivyo, utumizi wa Mitandao ya mawasiliano (Internet) kwa kujifunza na kufanya tafiti za masomo yako au maudhui zenye tija, basi uzuri wa kukamilisha sifa yako ya Uwislamu ni kufanya uchunguzi huo, pasi na kupindukia mipaka.
Hali kadhalika, mambo ambayo ni wajibu kwako kuyatenda au kujiepusha kuyatenda, basi uzuri wa kukamilisha sifa yako ya Uwislamu ni kuyatenda mambo hayo, kama kukemea maovu unapoyaona yanatendwa na ikawa una uwezo wa kuyakataza.
Ni wajibu wako vile vile, kujiepusha yasiyokuhusu, kama kudadisi dadisi mambo ya watu, kama udaku na umbea; kwani uzuri wa kukamilisha sifa yako ya Uwislamu ni kujiepusha na mambo hayo. Mwenyezi Mungu Anajua zaidi.

69. Tisa: Imepokewa kutoka kwa ‘Umar
رضي الله عنه akisema: Amesema Mtumeصلي الله عليه وسلم : “Haulizwi mtu kwa nini amempiga mkewe” [Yaani asiulizwe Mume kwanini amempiga mkewe; kwani kumuuliza ni kutaka afichue siri za nyumbani kwake.] Ameipokea Abu Daud na wengine.[Amesema al-Albani: Hadithi hii ni dhaifu]
NYONGEZA: Yaani msimuulize mtu sababu ya yeye kumpiga mkewe; maana kumuuliza ni sawa na kumtaka afichue siri za kwenye ndoa, jambo ambalo ni wajibu kuzisalia kuwa siri ya watu wawili na Mola wao. Kwani kutaja hadharini siri za ndani ya ndoa ni haramu juu ya wote wawili: mume dhidi ya mke na mke dhidi ya mume. Ama pale itapohitajika kutajwa sababu hiyo, kama vile mbele ya qadhi, ambako mwanamke amefungua kesi dhidi ya mumewe, basi mume anaweza kutaja sababu za kumpiga mkewe, endapo atatakiwa kufanya hivyo, ili haki itendeke. Vivyo hivyo, mwanamke anaweza kumshitaki mumewe kwa wazee wa mume, iwapo anahisi anamuonea na kumnyanyasa, ili wazee wake wamwite na kumonya. Vivyo hivyo anaweza kumshitaki kwa wazee wake yeye. Ama kutoka hadharani na kusema siri za ndani haifai. Na Mume hana leseni ya kumpiga mkewe, bila ya sababu ya kisheria, na baada ya kuishiwa na busara. Na papo, si kumpiga kwa kumuumiza, wala kumnyanyasa.
YALIYOMO NA YATOKNAYO/
1. Dalili na Ishara ya uzuri, unyoofu na ukamilifu wa Uwislamu wa Mtu ni kutojiingiza katika mambo yasiyokuwa na faida naye, wala dharura ya kujiingiza.
2. Dalili na Ishara ya ubaya, udhaifu na upngufu wa Uwislamu wa Mtu ni kupoteza wakati katika mambo yasiyokuwa na faida naye, Si Duniani wala Si Akhera.
3. Wajibu wa Mwislamu kujishughulisha na yenye maslahi na manufaa naye, Duniani na Akhera.
4. Wajibu wa Mwislamu kujiepusha yenye madhara naye, duniani na Akhera.
5. Uharamu wa Unabe (Udaku), Umbeya, Usabasi, Uchochezi, Ufitinishaji na Upekupeku wa mambo ya watu.
6. Umuhimu wa kuutumia Wakati katika mambo yenye Faida na Masilahi mema, yanayoendana na Radhi za Mwenyezi Mungu. Yaani Wakati ni Bidhaa adimu sana. Usiipoteze bure.
7. Utukufu wa Nidhamu ya Uwislamu katika kujenga Jamii Bora, yenye kuishi kwa Salama, Amani, Utulivu na maelewano mema.
8. Uwislamu haukubali Uvivu, Ubwete wala uzembe na Ulegelege.
9. Ufasaha wa Mtume صلى الله عليه وسلم katika kutumia maneno machche, lakini ni jumuifu katika maana zake.
10. Uharamu wa kutoa siri za nyumbani baina ya mume na mke asi na dharura.
11. Ndoa ni Fungamanisho Takatifu la watu wawili; chini ya Jina la Mwenyezi Mungu; hivyo wajichunge na wasiohusika na Fungamanisho hilo.
12. Mke ni AMANA ya Mwenyezi Mungu kwa mume, hivyo ni wajibu kwa Mume kumcha zaidi Mwenyezi Mungu katika fungamanisho zake ni mkewe.
13. Mke ni kitulizo cha moyo cha Mume, hivyo ni wajibu kwake zaidi kwenda naye polepole na kumtuliza.
14. Wajibu wa wanandoa kuvumiliana kwa makosa madogo madogo, na hasa Mume kwa mkewe; kwani kuwekwa katika nafasi ya Kiogozi wa Ndoa, hakumaanishi leseni ya kufanya yasiyokubalika kwa Allah.
15. Kujuzu kumpiga mke, pigo hafifu, pasipo kumuumiza, endapo amekubuhu kwa utovu na jeuri.
16. Wajibu wa Mume kumtimizia Mkewe haki zake zote, ili kumnyima visingizio vya utovu na jeuri.
17. Wajibu wa wana-ndoa kujichunga katika mahusiano yao ya Ndoa, kwani – kama watu wa nje hawayajui ya andani- Mwenyezi Mungu anayajua na kuyaona kila dakika.
18. Uharamu wa kudadisi na kupekua pekua mambo ya wana-ndoa, pasi na dharura ya kutakiwa kufanya nivyo- tena kwa wanaohusika tu: Wazazi na Mahakama.
وبالله التوفيق
الحقير عبد القادر شريف آل الشيخ

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ambacho ni tafisri kamili ya
رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي
kilicho tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir Shareef.
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye Whatsup na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com
Hadithi za Leo, Alhamisi, tarehe 8 Mfungo Nane, 1437, sawa na 18 February, 2016.
KUHUSU KUMCHA MWENYEZI MUNGU.
SEHEMU YA KWANZA.
6-Mlango wa Uchamungu
Amesema Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالي :-
1. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu (al-‘Imran:102)
2. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama muwezavyo(al-Taghabun:16) [aya hii inafafanua vyema zaidi yaliyokusudiwa kwenye aya ya mwanzo]
3. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno yaliyo simama sawa(al-Ahzab:70)
Aya zinazo husiana na kumcha Mungu ziko nyingi na zinajulikana sana.
Kadhalika, Amesema Mwenyezi Mungu:سبحانه وتعالي ) ):-
4. Na mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, basi humtengenezea njia ya kutokea, na humruzuku kwa njia asiyo itazamia (al-Talaq: (2-3)
5. Mkimcha Mwenyezi Mungu Atakupeni kipambanuo, na Atakufutieni makosa yenu na Atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye faadhila kubwa (al-Anfal: 29).
Kuna Aya nyingi kuhusu maudhui ya mlango huu. Ama kuhusu Hadithi:-
70. Kwanza: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه akisema: Aliulizwa Mtume صلي الله عليه وسلم : “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Ni yupi ndiye mbora wa watu wote?” Akasema:
“Mwenye kumcha zaidi Mwenyezi Mungu”
Wakasema: “La. Hatukuulizi kuhusu ubora wa aina hiyo” Akawajibu:
“Basi ni Mtume Yusuf; mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu; mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kitukuu cha Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kinying’inya cha Kipenzi cha Mwenyezi Mungu (Ibrahim)”
Wakasema: “La. Hatukuulizi kuhusu ubora wa aina hiyo” Akasema:
“Kwa hivyo, mnaniuliza kuhusu koo za Kiarabu!? [kama ni hivyo] Basi aliyekuwa mwema wao, enzi za Ujahiliyya [Enzi za upotofu, kabla ya kuja Uwislamu] ndiye mwema wao, enzi za Uwislamu, iwapo atajifunza mambo ya Dini” Muttafaq ‘alayhi.
71. Pili: Imepokewa kutoka kwa Abu Sa’id al-Khudriyy رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume صلي الله عليه وسلم :
“Dunia ni tamu na inavutia. Na Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالي Atakukabidhini uwongozi Wake [kutoka kwa walio kutangulieni] ili Akujarubini mtafanya nini.
Hivyo basi, jichungeni na Dunia na jichungeni (tahadharini) na wanawake; kwani fitina ya mwanzo waliojariabiwa nayo wana wa Bani Israel, ilikuwa kupitia kwa wanawake” Ameipokea Muslilm.
UFAFANUZI.
Kumcha Mwenyezi Mungu maana yake KUJKINGA Naye, kwa kumuogopa na kumchelea. Neno تقوى linatokana na Qi! Na hilo Qi lintokana na Wiqaya. Na Wiqaya maana yake KUJIKINGA. Hivyo, kumcha Mwenyezi Mungu ni kujikinga naye; kwa kujiwekea Hifadhi, au Kizuwizi cha kuepuka ghadhabu Zake, ili upate Radhi Zake na Rehema Yake. Na hayo hayapatikani isipokuwa kwa kutenda Aliyokuamrisha uyatende na kuepuka Aliyokukataza kuyafanfya; kwa KUMTII YEYE TU.
Na hiyo ndiyo maana ya Amri ya Mwenyezi Mungu katika Surat aal-‘Imraan: 102 “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, Allah, kama ipasavyo; wala msife ila nanyi ni Waislamu!” Yaani JIKINGENI NAYE KIKOMO CHA UWEZO WENU WA KUJIKINGA NAYE! Na hakikisheni kuwa hamfi ila na nyinyi ni Waislamu.
YALIYOMO NA YATOKANAYO.
1. Wajibu na Dharura ya kushikiamana na kamba ya Kumcha Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى kwa kauli na vitendo, nyakati zote.
2. Kumcha Mwenyezi Mungu ni Kijikinga Naye, na kujikinga na Mwenyezi Mungu ndio njia pekee ya kuokoka kwenye shida na matatizo.
3. Mwenye kushikamana na Taqwa kwa Allah, peke Yake, hufunguliwa njia mbali mbali za kuondokana na shida zake, na humpa riziki yake, kwa njia za ajabu ajabu, pasipo kutazamia.
4. Amchae Mwwenyezi Mungu, kikomo cha uwwezo wake, basi Mwenyezi Mungu hujaza Nuru katika moyo wake na akili yake, akawa hahisi wala haioni maovu, katika maisha yake; kwani giza na mwangaza huwa waziwazi mbele yake.
5. Kumcha Mwenyezi Mungu ndio fidia ya makosa na raba ya madhambi ya mchamungu.
6. Asiyemcha Mwenyezi Mungu hawezi kuwachelea watu! Yaani Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu hawezi kuwadhulumu watu wala kuwafanyia uovu wowote; maana anajuwa kuwa Mwenyezi Mungu yupo mbele yake tu.
7. Mcha Mungu Si mtovu.
8. Utukufu na Ubora wa viumbe vyote ni Ucha Mungu tu. Amchae Mwenyezi Mungu zaidi ndiye mbora zaidi wa wengine.
9. Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu huwa na kheri nyingi duniani, na daraja kubwa Akhera.
10. Nabii Yusuf –alipewa utume na kuwa mja mwema- akiwa kitukuu cha nne cha Nabi Ibrahim عليهم السلام
11. Vizazi vinastahiki Heshima na Utukufu wa Wazazi wao na Koo zao, iwapo wao wenyewe, vile vile ni wacha Mungu.
12. Vizazi vya Mawalii wa Mwenyezi Mungu na Vitukuu vya Mtume صلى الله عليه وسلم vinastahiki heshima, zaidi maalum, katika jamii, endapo wao wenyewe wanafuata nyayo za mababu zao watukufu.
13. Tabia na Hulka njeme za za Koo zilizopita, zinaendelea kuwa Tabia na Hulka njema katika Uwislamu, chini ya udhibiti wa Sharia za Mwenyezi Mungu.
14. Dunia ni nogefu na inavutia; lakini ni danganyifu. Ni kama mazigazi (saarabi) ya jangwani. Usidanganyike nayo!
15. Mtihani mkubwa wa kuonjwa mwanadamu hupitia kwa wanawake; ni chambo chema cha Shetani kupotosha watu: Wanaume na Wanawake; hata wenyewe kwa wenyewe.
16. Wajibu wa kujiepusha na mambo yanayo changamsha matamanio ya mwili yanayoweza kupelekea Zina.
17. Uharamu wa Zina haupo kwenye kitendo chenyewe tu, bali hata katika vinavyo kusogeza kuendea Zina. ولا تقربوا الزنا “Msisogelee Zina!”
18. Umuhimu wa kujifunza kutokana na watu waliotuganulia katika maafa yaliyowafika katika matendo yao. Asiyeangalia matukio hana ajifunzalo.
19. UCHA MUNGU NI NGAO! JIKINGE KWAYO!
وبالله التوفيق
الحقير عبد القادر شريف آل الشيخ
Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ambacho ni tafisri kamili ya
رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي
kilicho tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir Shareef.
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye Whatsup na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com

No comments:

Post a Comment